Wenyeji Mlima Elgon waanza kupata afueni ya usalama – Taifa Leo

0
28


Na MWANGI MUIRURI

NI ghasia ambazo zilisababisha vifo vya watu 300 huku wengine 60,000 wakifurushwa kutoka kwa makazi yao katika mradi wa mashamba wa Chepyuk katika Kaunti ya Bungoma na ambapo Sabaot Land Defence Force (SLDF) lilidaiwa kutekeleza ukatili huo.

Lakini sasa hali inaonekana kudhibitiwa na usalama kurejea ambapo kambi za wakimbizi 28 zilizokuwa zimechipuka kwa sasa zimefungwa na raia kurejea katika maisha yao ya kawaida.

Hasa maeneo yaliyoathirika zaidi ni Kaberos na Kapkwes katika tarafa ya Cheptais.

Hali hiyo ilihusishwa na uchochezi wa wanasiasa ambapo mtandao wa wahalifu walifadhiliwa kuwaua wenyeji.

Waliokuwa walengwa katika sakata hiyo ya umwagaji damu kiholela ni wale waliodaiwa kunufaika na mashamba katika eneo hilo licha ya kuorodheshwa ‘kiharamu’ kama wageni.

Bi Lilian Chepkelei akiwa na mtoto wake mwenye umri wa miezi sita katika eneo la Chepyuk. Picha/ Mwangi Muiruri

Wanasiasa wakuu serikalini walidaiwa kufahamu kuhusu uhalifu ulioshamiri ambapo wenyeji – hasa wanawake wakongwe na watoto – walihangaika kwa sababu ya kudorora kwa usalama.

Ni hadi wakati ule Waziri wa Usalama wa Ndani Dkt Fred Matiang’i aliamrisha kuwa hali hiyo ikomeshwe na akamwaga maafisa tele wa kudumisha usalama eneo hilo ambapo hali ilianza kuimarika.

Katika ghasia za 2007 ambapo SLDF ilikuwa ikiwatoza wenyeji ushuru haramu, kuua kiholela na kudhibiti eneo hilo la Mlima Elgon kiharamu, aliyekuwa Waziri wa Usalama, John Michuki aliwajibikia kero hiyo na ambapo aliomba usaidizi wa kikosi cha wanajeshi kuwindana na wahalifu hao.

Matokeo yalikuwa mwaka wa 2008 aliyekuwa amefahamika kama kamanda wa kikosi hicho, Wycliffe Matakwei kupigwa risasi na kuuawa na ndipo hali ya utulivu ikarejea. Alitajwa kuwa ni naibu kamanda wa SLDF.

Mradi huo wa mashamba umekuwa na utata kwa kuwa kuna jamii kadhaa ambazo zilituzwa vipande vya ardhi katika eneo hilo ambalo lilikatwa kutoka Mlima Elgon na kugeuzwa kuwa makao na kilimo.

Kuna jamii za Soi na Dorobo, Teso na Bukusu na pia wengine kutoka jamii zingine kadhaa na ambapo hadi sasa hakujawahi kuwa na makubaliano kamili ya ni kina nani hasa wanafaa kunufaika na mashamba hayo, huku mitandao ya unyakuzi ikitajwa kujumuisha baadhi ya viongozi wanaozidisha uhasama.

Mwaka wa 2007, mradi huo wa Chepyuk ulitazamiwa kugaiwa kwa walengwa ili kuzima mauaji hayo na ndipo serikali ikatoa ratiba ya kugawa vipande vyote 4,000 ambavyo vinajumuisha sakata hiyo.

Katika harakati za kutoa orodha ya ugavi, iliibuka kuwa ni ploti 1,772 ambazo ziliwekwa wazi kupeanwa, watu 2,228 wakiachwa nje na ambapo walidaiwa kufurushwa kutoka umiliki wao na mtandao huo wa unyakuzi mashamba.

Ni katika hali hiyo ambapo mawaziri Dkt Matiang’i na Waziri wa Ardhi Faridah Karoney wanashabikiwa kama waliolivalia njuga suala hilo na kuamrisha mikakati ya kudhibiti hali itekelezwe.Source link