Tanzania na Afrika Kusini kuimarisha mahusiano ya kibiashara

0
18


Haki miliki ya picha
IKULU, TANZANIA

Image caption

Rais John Pombe Magufuli na Cyril Ramaphosa wameahidi kuwezesha uwekezaji kushamiri kwenye mataifa yao.

Rais John Pombe Magufuli na Cyril Ramaphosa wa Tanzania hii leo wametangaza kuendelea kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kirafiki baina ya mataifa hayo mawili wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika, SADC.

Magufuli na Ramaphosa pia wamewakaribisha wafanyabiashara wa Tanzania na Afrika Kusini kuwekeza kikamilifu kwenye nchi hizo.

Ramaphosa yupo ziarani nchini Tanzania tangu Jumatano usiku, na hii leo amefanya mazungumzo na mwenyeji wake Magufuli Ikulu ya Magogoni na baadae wakahudhuria kongamano la wafanyabiashara wa nchi hizo mbili katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere.

“Kupitia Rais Ramaphosa, nimewaalika wafanyabiashara wa Afrika Kusini kuja kujenga viwanda nchini ikiwemo viwanda vya kusindika mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi, viwanda vya madawa na viwanda vya kuchakata na kuongeza thamani kwenye madini,” amesema Rais Magufuli.

Magufuli amesema vivutio vya uwekezaji nchini Tanzania ni vingi, huku akiangazia zaidi viwanda vya dawa na vifaa tiba, madini na utalii.

“Tanzania tumepewa fursa na shirika la kimataifa la Global Fund kununua dawa na kusambaza katika ukanda wote wa SADC lakini cha kusikitisha ni kuwa zaidi ya asilimia 98 ya manunuzi hutoka nje ya Afrika,” amesema Magufuli.

Kwa upande wake, Rais Ramaphosa amewakaribisha wafanyabiashara kwenda kuwekeza Afrika Kusini na kusema kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha kuna mazingira mazuri ya kufanya biashara.

Haki miliki ya picha
IKULU, TANZANIA

Pia, Ramaphosa ameendelea kusistiza kuwa nchi yake iko tayari kutumia fursa ya kujifunza lugha ya Kiswahili licha ya kuwepo kwa lugha mbalimbali zinazozungumzwa nchini mwake.

Mei mwaka huu, Magufuli na Ramaphosa walikubaliana juu ya Tanzania kupeleka walimu wa Kiswahili nchini Afrika Kusini.

Ziara ya Ramaphosa inakuja siku chache kabla ya Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi Wanachama wa SADC utakaofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.

Kesho, Ramaphosa anataraji kutembelea kambi ya Mazimbu mjini Morogoro ambapo wapiganaji wa ANC walikuwa wakikaa na kupatiwa mafunzo na serikali ya Tanzania.

“Tunatambua Rais Magufuli anakuwa mwenyekiti wa SADC, nimemhakikishia kwamba tutampatia ushirikiano wote katika kudumisha amani, biashara na ushirikiano baina yetu.”

Biashara baina ya Tanzania na Afrika Kusini imeongezeka kutoka dola bilioni 1.11 mwaka 2017 mpaka bilioni 1.18 mwaka 2018.

Kampuni za kutoka Afrika Kusini zimewekeza kiasi cha dola milioni 803.15 nchini Tanzania.

“Kwa mwaka 2018, Tanzania ilipeleka bidhaa za chakula za kiasi cha dola milioni 743.02 kwenda Afrika Kusini, na kuagiza bidhaa za kiasi cha dola milioni 437.2 kutoka Afrika Kusini mwaka jana.”Source link