Serikali Kenya yaanza msako wa kukagua wanaume wasiotahiriwa, Yadaiwa ni vita ya kupambana na maambukizi ya Ukimwi

0
54


Serikali nchini Kenya katika kaunti nne za eneo la Nyanza, imeanza kukagua wanaume kwa vitendo ili kubaini kama wametahiriwa au laa!.

Wizara ya Afya nchini humo imesema uchunguzi huo unaendeshwa na Shirika la Wanaume la Kutahiri kwa Hiari (VMMC) unalenga kupambana na ongezeko la maambukizi ya virusi vya Ukimwi.

Ukaguzi huo ulioanza Jana Jumatatu Julai 22, 2019 unalenga kufahamu idadi ya wanaume waliotahiriwa na wale wasiotahiriwa katika kaunti za Homa Bay, Kisumu, Siaya na Migori. Na utadumu kwa miezi mitatu.

VMMC wamesema kuwa watatumia njia ya mahojiano ya kawaida kwa wale ambao hawatapenda kukaguliwa, hii ni kutokana na mila na desturi za jamii husika.

Huduma za VMMC zilianza kutolewa katika eneo la Nyanza mwaka wa 2008 kabla ya kueneza huduma hizo hadi maeneo mengine nchini Kenya.

Kwa mujibu wa Dkt. Akeche, utafiti wa kukagua wanaume ulianzia Nyanza na umefadhiliwa na serikali ya Marekani  na una lengo la kupambana na maambukizi ya virusi vya VVU .

Wakati VMMC ilipoanzisha mpango wa tohara, idadi ya maambukizi ya HIV yalianza kupungua pamoja na idadi ya wanaume waliofika kutahiriwa. Utafiti huu utasaidia kufahamu iwapo bado kuna wanaume ambao hawajatahiriwa, Wanaume wenye umri wa juu ambao pia wapo hatarini kuambukizwa ukimwi wamekuwa wakikwepa tohara. Hii itakuwa fursa ya kufahamu idadi yao na kuwashawishi kukumbatia kisu cha ngariba,” amesema Dkt. Akeche na kudai kuwa wanaume kati ya umri wa miaka 19 hadi 29 ndio wamekuwa wakifika kwenye kliniki zao kutahiriwa.

Dkt. Akeche amesema matokeo ya uchunguzi huo yatasaidia kukadiria bajeti ya kufadhili vita dhidi ya maambukizi ya ukimwi eneo la Nyanza hasa kaunti ya Homa Bay ambayo inaongoza katika orodha ya maambukizi nchini Kenya kwa asilimia 26.

Chanzo: Taifa Leo – Serikali kukagua wanaume kubaini ikiwa wametahiriwaSource link